SERIKALI YAPOKEA GAWIO LA SH. BILIONI 17 KUTOKA CRDB

 

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amepokea gawio la Sh. bilioni 17 linalotokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya Benki ya CRDB.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dk. Ally Laay alimkabidhi Dk. Mpango hundi kifani ya fedha hizo jijini Dodoma leo Agosti 10,2020 mbele ya baadhi ya viongozi na mawaziri mbalimbali wa taasisi na mashirika ya umma yenye hisa ndani ya Benki ya CRDB na Menejementi yake.

Akizungumza katika hafla hiyo Dk. Mpango aliipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa gawio kwa serikalini na kupata matokeo mazuri ya fedha mwaka 2019 ambayo yamepelekea kuongezeka kwa gawio kwa Wanahisa  ikiwamo Serikali.

“Ongezeko hili la gawio ni kiashiria tosha kwa serikali kuwa benki hii inazidi kuimarika kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea na jambo linalowapa moyo watanzania na wawekezaji kuwa benki inatoa huduma bora katika jamii,” alisema Dk. Mpango.

Dk. Mpango alisema fedha zilizopatikana kupitia gawio hilo zitakwenda kusaidia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeianisha katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2020/2021.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Vijana, Jenista Mhagama alipongeza mifuko ya jamii ya PSSSF, NSSF na ZSSF kwa uwekezaji ndani ya Benki ya CRDB huku akiwataka viongozi wa mifuko hiyo kutumia gawio lalilopata kuboresha utendaji kazi ili kunufaisha wanufaika wa mifuko hiyo.

Serikali ndio mwanahisa mkubwa ndani ya Benki ya CRDB kutokana na kuwa na umiliki wa asilimia 21 kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA kushirikiana na Serikali ya Denmark, huku taasisi na mashirika ya umma yakiwa na umiliki wa hisa za asilimia 17.1.

Comments