Mfahamu Malkia Nzinga wa Angola na Kiboko ya Wareno!
Nzinga alizaliwa katika familia ya kichifu, baba yake alikuwa Chifu wa Ufalme wa Ndongo, Chifu aliyempenda mtumwa wake kwa dhati, akamfanya kuwa mke wake, akazaliwa mtoto wa kike, jina lake akaitwa Nzinga kwa sababu kitovu kilimzingira shingoni wakati wa kuzaliwa, Nzinga mtoto wa mtumwa akaja kupambana na biashara ya utumwa hadi Wareno wakamnyoshea mikono, Nzinga akaingia kwenye rekodi ya wanawake wa shoka Duniani.
Mama yake Nzinga aliitwa Kengela ka Nkombe na baba yake Chifu Kilombo wa Ndongo. Nzinga na baba yake walikuwa pete na kidole kama ilivyokawaida kwa watoto wengi wa kike na baba zao. Nzinga alipewa mafunzo ya kijeshi katika umri mdogo na muda mwingi aliambatana na baba yake katika shughuli mbalimbali za kiserikali. Ukaribu aliokuwa nao na baba yake ulimpa fursa ya kukutana na wageni mbalilmbali waliofika pale Ikulu hadi akajifunza kuandika na kuzungumza Kireno vizuri.
Wareno walifika Angola tangu karne ya 15 kufanya biashara ya watumwa. Nchi ilichafuka balaa. Chifu alijaribu kila mbinu kumaliza migogoro hadi akafa bila kufua dafu. Alikufa zake mwaka 1617. Kaka yake Nzinga akapewa Uchifu lakini ukamshinda kwa sababu aliwekeza nguvu katika kulinda nafasi yake ya uchifu kwa kuwaumiza dada zake badala ya kukomboa nchi yako. Huyu jamaa alihofia sana mtoto wa Nzinga kuja kumpindua hivyo akaagiza watu wamuue, dogo akafa bila hatia, kisha Nzinga naye akakamatwa na kuharibiwa kizazi ili asijekuzaa tena.
Kitendo hicho kilimuumiza sana Nzinga na kuondoka zake kuelekea Matamba. Akiwa huko Matamba Nzinga aliendelea kujifunza mbinu za kivita ili siku moja aje kumpindua kaka yake. Mungu si athumani kaka yake nchi ikamshinda, Wareno wanamsulubisha kwelikweli, watu wake wanasombwa kupelekwa utumwani kila siku, viongozi waandamizi wanachinjwa kila siku. Ureno ilipopata Gavana mpya, Chifu akaona hapa suluhu ni kwenda kuomba maridhiano na Mreno! Tatizo lugha haipandi. Akamuomba dada yake Nzinga akamuwakilishe.
Nzinga alipopata taarifa kutoka kwa kaka yake hakuwaza mabaya aliyomfanyia badala yake alifurahi na kwenda kumsaidia kaka yake kwa maslahi mapana ya nchi. Mwaka 1622, Nzinga alitua Luanda tayari kwa mazungumzo na Gavana Dom João Correia de Sousa. Katika mkutano ule viongozi wa Ndongo wote walipiga pamba za kizungu, lakini Nzinga akala zake pamba za asili ili kuwaonyesha wazungu kwamba utamaduni wao siyo wa kishenzi kama walivyotufundisha.
Wakati Nzinga anaingia ukumbini alikuta Gavana ameketi kwenye kiti na yeye kutakiwa kukaa chini ili mazungumzo yaanze. Hi indo ilikuwa tabia ya Wareno kuwachukulia waswahili watu wa hadhi ya chini, watu wenye hadhi ya kukalia mawe, mikeka, magogo na kuchuchumaa huku mzungu akiketi kwenye kiti cha mfalme. Nziga akasema upuuzi gani huu. Akamuita askari wake mmoja, akainama chini, Nzinga akaa juu yake, mazungumzo yakaanza.
Nzinga alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kuzungumza hadi Wareno wakamuelewa, vurugu zikaisha, Mreno akaondoa majeshi yake kwenye ardhi ya Ndongo na kuitambua Ndongo kama ardhi huru. Akakubali kufungua biashara na Wareno na akakubali kubatizwa na kuwa mkristo. Mama wa ubatizo akawa mke wa Gavana, akaitwa Dona Anna de Sousa jina la mke wa Gavana. Nziga akamaliza vita iliyomshinda baba yake na kaka yake.
Kaka yake alimgeuka na kumwambia amemsaliti kwa kushirikiana na Wareno hadi kukubali kubadili dini na kubatizwa. Nzinga akasema ukitaka kummaliza adui yako msogeze karibu. Hata hivyo makubaliano waliyoingia Mreno hakuyafuata kwa sababu iliibuka vurugu kubwa kati ya dola ya Ndongo na dola ya Imbangala. Wareno wakaendeleza kuikalia Ndongo na kuendelea kuwakamata waafrika na kwenda kuwauza utumwani.
Mwaka 1624 kaka yake alikufa kifo cha ghafla na Nzinga kukalia kiti cha uchifu, akawa Malkia wa Ndongo, wakasema Nzinga ndo alisuka mpango wa kumuondoa kaka yake maana alitia aibu.Nzinga akawambia huwa siui kisirisiri nadhani muziki wangu mnaujua.Nzinga alipata upinzani mkubwa sana hadi kutimuliwa.Nzinga alichokifanya ni kumteka Malkia wa Dola ya Matamba na jeshi lake, akajitangaza Umalkia wa Matamba na kufanya maandalizi ya kurudi kwenye kiti chake kule Ndongo na kwelia akarudi na kujitangazia Umalkia wa Ndongo na Matambara.
Wananchi wakamwambia kwanza wewe huna sifa hata moja ya kutawala kwa sababu mlikuwa watoto wa mtumwa. Nzinga akawambia mtumwa likuwa mama, siyo baba. Alipowashinda kwa hoja hiyo, wakaja na hoja ya jinsia, kwamba mwanamke hana uwezo wa kutawala. Nzinga alivyoona hawamuelewi mwaka 1640 akaamua kuwa mwanaume. Akaanza kufanya yale waliyofanya wanaume. Binti akaongoza vita, alishika silaha na kupigana kwa ujasiri mkubwa sana hadi wanaume wakanyosha mkono.
Mwaka 1641 majeshi ya Dutch Empire, yakishirikiana na Dola ya Kongo, waliuteka mji wa Luanda. Nzinga akatuma ujumbe wa kidiplomasia wayamalize. Wakakaidi, mapigano yakaendelea. Mwaka 1947 Nzingha akawashinda Wareno. Binti alipandikiza maspy kibao kwa Wareno akiwemo dada yake ambaye alikuja kukamatwa na kutupwa Mto Kwanza,za ingawa wenyewe wanasema dada alitoroka na kukimbilia Namibia.
Mwaka 1656, baada ya kukutana na wakapuchini wamisionari wakamwambia akikubali kuwa mkristo Papa ataitambua nchi yake na hakuna atakayewasumbua. Nzinga akakubali, akaokoka kwa mara ya pili. Novemba 24, 1657, Wareno walinyosha mikono, wakaiachia Ndongo na ardhi kurudhishwa kwa Malkia kupitia maktaba uliosaniwa huko Lisbon na King Pedro VI. Bada ya vita kuisha mama alianza kujenga taifa lake upya lililokuwa limeharibika sana kwa sababu ya vita ya muda mrefu.
Nzinga akafariki akiwa na umri wa miaka 81.
TAZAMA VIDEO HAPA>>>
Mfahamu Mzee Mkapa: Rais Aliyeleta Ukombozi wa Kifikra na Uchumi; Waelewa Wakagonga Cheers; Wajuaji Wakamtukana!
Mzee Mkapa aliingia madarakani nchi ikiwa imedumaa kiuchumi, akatawala kwa falsafa ya “Huwezi kupata maendeleo bila kubadili fikra” akasisitiza watu wafikiri kwa bidii hadi nchi ikakombolewa, waliomuelewa wakala bata, waliozembea kufikiri aliwatukana hadharani wakamuita mbabe, dikteta na mwizi wa mali za umma kwa sababu ni hulka ya binadamu kushughulika na madhaifu ya mtu kuliko mazuri yake, hata Mungu huwa tunamfanyia hivyohivyo pale tunapotumia muda mwingi kumuomba vitu ambavyo hatuna badala ya kumshukuru kwa vitu vingi alivyotupatia.
Kuna mwalimu aliingia darasani na karatasi nyeupe zenye doa katikati, akawagawia wanafunzi kisha akawaambia kila mmoja alezee alichoona kwenye karatasi; wote walizungumzia doa limechafua karatasi. Mwalimu akawauliza ina maana hakuna aliyeona sehemu nyeupe kwenye karatasi?” Mliiona isipokuwa katika jamii ya walimwengu kosa moja litosha kufukuza mke. Maana yake ni kwamba ukimuangalia Mkapa kwa macho ya wanafunzi huwezi kuona meupe, utaishia kuona madoa yake tu.Karibu tuangalie meupe 13 kutoka kwa Mkapa!
Moja: Urais wa Mkapa ni message kwa wazazi wanaowapangia watoto wao vitu vya kusomea waache, Mungu aliishawapangia makubwa! Huyu Mkapa aliyezaliwa Jumamosi ya tarehe 12 Novemba 1938 kijijini Lupaso Masasi baba yake alitamani awe padre wa jimbo akawa rais wa nchi. Najua baba alitamani hivyo kwa sababu aliishaonja utamu wa kumtumikia Mungu. Siunajua mzee alikuwa katikista pale Ndanda Mission, Masasi?
Basi bwana Ben akasoma msingi, sekondari hadi chuo kikuu. Msingi alisoma Lupaso na baadaye alikwenda seminari ya Junior Benedictine (Kigonsera) kuutafuta Upadre ili kutimiza ndoto ya baba yake, lakini Mungu akasema wewe ni Rais wa nchi, siyo Padre, ondoka upesi, Mkapa akarudi zake Ndanda kuendelea na Middle School, alivyomaliza darasa la kumi akataka kwenda uaskari, Mungu akasema wewe ni Rais wa nchi siyo askari,songa mbele, Mkapa akalisongesha hadi Pugu, enzi hizo Pugu inaitwa St.Francis College.
Akiwa Pugu alindika historia ya kufundishwa na Nyerere kisha wakatawanyika, Nyerere akaelekea kutafuta uhuru nchi, Mkapa akaelekea kutafuta uhuru wa kichwa nchini Uganda, akapiga miaka yake mitatu pale Makerere University, 1962 akatoka na jiwe la Lugha na Fasihi, akarudi nchi wakakutana tena na Nyerere akiwa na uhuru mkononi na yeye elimu kichwani,akapewa Ukatibu Tawala Dodoma, vyeo vikaanza kumgombania, mara balozi, mara mbunge, mara waziri wazazi wakashuhudia uwaziri wa aliyetakiwa kuwa padre, halafu wakaondoka zao duniani bila kusubiria urais wa mwanao!
Mbili: Mkapa aliamini Tanzania inahitaji strong institutions not strong men ili kutoka mavumbini ndo maana akaanzisha taasisi kibao; palipo na umasikini alifungua TASAF maskini wakaanza kula na kushiba; palipokosa uhakika wa matibabu alifungua bima ya afya watu wakawa na uhakika na afya zao, palipojaa rushwa alianzisha TAKURU kuitokomeza; waliokosa uhakika wa kwenda vyuo vikuu alianzisha Bodi ya Mikopo maskini wakaingia vyuo vikuu kwa mbwembwe na ushamba ndani yake, kama unavyojua tena maskini akipata ghafla kinachotokea!
Palipo na upotevu wa mapato, alianzisha TRA, mapato yakaongezeka karibu mara tatu kutoka dola 612,587 hadi dola 1,796,862 kwa mwezi, akawakuna mabeberu hadi kupunguza deni la Tanzania; ili kulinda rasilimali za wanyonge alianzisha MKURABITA kurasimisha rasilimali za wanyonge ardhi yao ikapata maana; ili kuvutia uwekezaji alianzisha TIC, wageni wakachangamkia fursa wazawa wakalala Mkapa akabaki kushangaa watanzania mko wapi?
Katika kuimarisha usalama wa nchi alianzisha TISS nchi ikawa na usalama wa uhakika, yako mengi sema usinichoshe, nisikuchoshe, tusichoshane kuyataja yote, kama vipi tafuta kitabu chake yamo yote! Kinaitwa My Life; My Purpose!
Tatu: Albert Einstein aliposema ukiwa na mawazo mafupi yasiyozidi mwaka mmoja panda mpunga, ukiwa na mawazo yanayoishia miaka kumi panda mti, ukiwa na mawazo marefu kupita miaka 100 panda elimu kwa watu wako, Mkapa alipanda elimu kwenye vichwa vya watanzania kwa sababu mawazo yake yalipitiliza miaka mia. Aliamini maendeleo huanzia kichwani. Kichwa kisipokaa vizuri utaitesa midomo yako kwa kuzungumza watu badala ya issues halafu ukiambiwa uache wivu wa kike unarusha ngumi.
Halafu katika kupanda elimu kwa watu wake Mkapa alishirikisha taasisi za dini sababu asingeweza kukweya mnazi kwa mkono mmoja. Akaamua kutoa majengo ya Mazengo Sec kwa waanglikana wakaanzisha St. Joseph University Dodoma, majengo ya Benki Iringa wakapewa wakatoliki wakafungua Ruaha University; majengo ya TANESCO Morogoro wakapewa waisilamu wakaanzisha Chuo Kikuu cha Kiislamu, majengo ya sekondari ya Magamba Rushoto wakapewa walutheri wakaanzisha Sebastian Kolowa Memorial University, vijana wetu wakamwagika vyuoni, elimu ya chuo kikuu ikawa kitu cha kawaida kwa sababu vyuo vikuu vilizagaa kila kona ya nchi kama mahindi ya kuchoma, full usanii, Mzee Magufuli alivipuruni, mashaka yakatanda kwa waliosoma huko itakuaje?
Nne: Mkapa aliuchukia umaskini kwa sababu palipo na umaskini chuki na wivu hutamalaki, maskini anaweza kupiga vibarua kutafuta pesa ya kumloga mwenzake kisa tu anamshahara wa ukatikista. Hili Mkapa alilishuhudia kwao jinsi mshahara wa baba yake ulivyowaumiza usiowahusu hadi kuwasababishi balaa familia ya kina Mkapa. Mwaka 1947 ulitokea ukame kijijini kwao, wanakijiji wakamleta mpiga ramli akasema mama yake Mkapa na bibi yake ndo walozi, walikula kisago hadi bibi akapoteza maisha. Unajua tatizo la umaskini unakimbilia kula ubongo ndo maana maskini hana hoja, anahaja.
Ili kuwapa ahueni maskini, Mkapa alifuta kodi ya kichwa iliyowatoa jasho wazee wetu, kuna wazee walishinda porini kuwakwepa askari mgambo. Maskini alivaa nguo zenye viraka katika nchi huru. Suruali la baba likiisha lilishona kaptura za watoto. Mzee alifuta hadi kodi ya baiskeli na mifugo ili kumpa ahueni maskini, halafu alidhibiti mfumko wa bei hadi maskini wakagonga cheers! Katika utawala wake kilo ya sukari tuliinunua kwa shilingi mia tano kwa muda mrefu!
Alitaka maskini wachape kazi kwani mtaji wa maskini ni nguvu zao. Alipenda kusema sisi ni maskini mfukoni lakini matajiri kichwani. Hatuwezi kuweka fedha mifukoni mwenu ila tutandaa fursa za kupata pesa alisisitiza. Mazingaombwe ya kujazana mapesa alimuachai Mzee Cheyo wa Bariadi. Alisema tunatakiwa kubadilisha maisha yetu au tutabadilishwa tutasombwa kama vile mawimbi.
Tano: Mkapa hakupenda kuabudiwa kabisa ndo maana alikataa kuitwa Mtukufu Rais kama walivyoitwa Mtukufu Al-Hassan Mwinyi na Mtukufu Daniel Arap Moi; alikataa picha yake kutumika kwenye sarafu, alikataa kuitwa daktari pamoja na kutunukiwa PhD kibao za heshima, hata barabara ya kwenda kwao imekuja kujengwa na Rais Magufuli, yeye aligoma. Hata huu uwanja wa mpira umekuja kuitwa kwa jina lake baada ya kuondoka duniani. Unaitwa Mkapa Stadium. Halafu yeye ndo aliujenga. Ni uwanja wa kisasa kweli kweli hadi Brazil wakaja kuweka kambi tukawaona akina Ricardo Kaka, Robinho Do Santos na Ruis Fabiano live.
Lakini pia Mkapa hakupenda kuonyeshwa kwenye TV mara kwa mara kama Moboutu Seseko wa Zaire ndo maana aliwashauri waonyeshe mambo ya maendeleo na changamoto za vijijini. Hata aliposaidia watu hakuhitaji kuitangazia dunia kama mnavyofanya nyie. Alitumia kanuni ya utoapo fanya kuwa siri ikiwezekana hata mkono wako wa kushoto usione! Soma Mathayo 6:3! Tujifunze kwa Ben.
Sita: Mkapa alikuwa msomaji mzuri wa vitabu ndo maana alijua mengi! Kutosoma vitabu ni kujiongezea janga la umaskini alipenda kusema Mkapa. Mbele ya Mkapa kama husomi na kufanya tafiti alikuona kenge. Waandishi wa habari wazembe walipata taabu sana enzi zake. Aliwaita wavivu wa kufikiri. Kufikiri sio kipaji ni tabia. Hotuba za Mkapa zilikonga nyoyo za wengi kwa sababu ya utamaduni wake wa kusoma sana. Enzi zake nchi ilikaa kimya kumsikiliza mwanaume akiongea. Aliongea kila mwisho wa mwezi. Mkapa aliargue hakushout! Mkapa alikuwa kama "library" inayotembea.
Halafu alikuwa na majibu ya kuudhi balaa hasa ukimuuliza swali lilitofautiana na fikra zake. Nakumbuka siku ya Mei Mos wafanyakazi walipomshambulia kwamba halindi ajira za wazawa alisema, “Mimi sijali rangi ya paka najali kama anakamata panya au la". Someni vitabu ili muendelee kupata maarifa. Maarifa ni nguvu kubwa zaidi ya vifaru. Unaweza soma hata vitabu vya Mpagaze, anza na Ukombozi wa Fikra, ukiishafunguliwa chukua Wasomi Huru Gerezani, piga namba hizi ujipatie kopi zako halafu tuendelee; Dar es Salam piga....Arusha piga 0744126082, Mwanza 0756179573, KAHAMA
0769006232, IRINGA ni Citymax bookshop 0753690907 na Songea
0712648387 na kwa soft copy 0753665484. Bei ya Soft copy ni 5,000 tu!
Saba: Nyumbani Mkapa atakumbukwa daima kama Rais aliyekuza uchumi, kujenga taasisi imara na kufanya makosa kwenye ubinafsishaji na uuzaji wa nyumba za serikali akafanya toba miezi nane kabla ya kufa kwake sababu kukosea ni ubinadamu kukiri makosa ni uungwana, lakini huko nje Mkapa atakumbukwa daima kama mpatanishi wa amani. Kenya Mkapa anakumbukwa kwa kutuliza lile sekeseke la Uchaguzi Mkuu mwaka 2007 liliondoka na roho za wapendwa wetu 1,000; Burundi nako, Mkapa alimaliza vurugu za warundi waliopigana bila sababu ya msingi na kufanya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia kwa Nkurunziza kuingia madarakani; Rwanda nako Mkapa aliwasaidia kuponya madonda ya mauaji ya kimbari!
Nane: Mkapa ndo alikuza uhuru wa habari ingawa washikaji zake wanamponda kwamba ndo aliua uhuru wa habari. Mkapa hakula chakula cha jioni kabla ya kusikiliza taarifa ya habari. Alisoma sa magazeti hadi barua za wasomaji na wakati mwingine aliwaagiza wasaidizi kuwatafuta waandishi wa barua zilizomgusa. Waandishi wengi wa Tanzania aliwaita wavivu wa kufikiri kutokana na aina ya habari walizoandika na maswali mepesi waliyomuuliza. Waandishi wengi waliuliza maswali ya kutafuta uteuzi. Mkapa amewahi kutangaza RTD na kuhariri magazeti ya chama pamoja na Daily News, alitumia jina la bandia kuwakosoa viongozi kupitia gazeti. Alijiita "Mwana wa Matonya! Lakini pia ndo mwanzilishi wa SHIHATA, yaani Idara ya Habari Maelezo ya leo. Mkapa amefariki muda mfupi baada ya kuangalia TV.
Tisa: Katika utawala wake Mkapa alikutana na majanga mazito yakamuimarisha badala ya kumdhofisha ndo maana hakuikimbia Ikulu. Mei 21, 1996, mwaka mmoja tu baada ya kuingia madarakani likatokea balaa la kuzama kwa meli ya MV Bukoba, mwaka uliofuta yaani 1997 mafuriko ya el nino yakavuruga nchi, Februari 13, 1998 sekeseke la mauaji ya mwembe chai likatia doa utawala wake, Oktoba 14, 1999 baba wa Taifa akaondoka duniani, Januari 27, 2001 mauaji ya Pemba yakautia doa tena utawala wake, Julai 4, 2001 makamu wa Rais Dr. Omar Ali Juma akaaga dunia! Lakini pia Mkapa anasema alikuwa na wasiwasi pale Rais wa Zanzibar Salmin Amour alipotaka kubadilisha sheria na kutawala kipindi cha tatu. Lakini baadaye waliyamaliza kiungwana.
Kumi: Mkapa aliumia sana aliposhambuliwa yeye binafsi na familia yake kwa mambo yaliyohusu nchi. Madai kwamba alimpendelea baba mkwe wa mwanaye katika kubinafsisha mgodi wa makaa ya mawe Kiwira yalimuumiza sana. Pia madai kuwa aliwapendelea NET GROUP solutions Ltd wakati wa kubinafisha TANESCO kwa sababu ya shemeji yake kulimuumiza sana pia. Anasema hata mashumbulizi aliyorushiwa kuhusu matumizi ya anwani ya Ikulu wakati yeye na mke wake walipochukua mkopo NBC kununua nyumba walikuwa wanaishi Ikulu hayakuwa fair. Hata suala la EPA lilimuumiza sana ingawa liliibuka tayari ametoka madarakani. Anasema Gavana wa Benki Kuu enzi hizo Daud Bilali ndo alimuingiza chaka.
Kumi na moja: Mkapa aliamini uwepo wa vyama vingi vya siasa unadhoofisha demokrasia ndo maana hakuvikubali kabisa vya vya siasa. Aliwahi kusema ushauri unatokana na nguvu ya hoja tutaupokea lakini ushauri unatokana hoja ya nguvu tutaikataa. Vyama vinavyosema vinajiandaa kuikomboa Tanzania ni wapumbafu, malofa, Tanzania iliishakombolewa na CCM. Wafanyabiashara wanaingia kwenye siasa ili kulinda maslahi, wasomi wanaingia kwenye siasa kutafuta safari na posho.
Kumi na Mbili: Umahiri wake katika kazi ulimsaidia Mkapa kuaminika sana. Mkapa amekuwa balozi Nigeria, waziri wa mambo ya nje mara mbili, enzi za Mwinyi na Nyerere 1977-1980 na enzi za Mwinyi 1984 -1990, amekuwa waziri wa Habari na Utamaduni 1980-1982, amekuwa waziri wa habari na utangazaji 1990-1992 na Waziri wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya juu 1992-1995.Hama hama zilivyozidi ilibidi watoto wao wabaki Marekani kukamilisha masomo yao. Hii dunia bwana, na wakati wewe mabosi wako wanakaa vikao kila siku kuangalia ni namna gani wakufukuze, Mkapa mabosi wake walimgombania.
Kumi na tatu: Mkapa aliipenda Afrika ndo maana hata baada ya kustaafu aliendelea kutupigania sana waafrika na siku zote alikuwa akiwashutumu mabeberu kwa hadaa zao dhidi ya Afrika. Alikuwa sehemu ya kundi hili la viongozi wa Afrika waliojipambanua kama kizazi kipya kinachotafuta suluhisho la matatizo ya watu wake kutoka ndani. Viongozi hao ni pamoja na Thabo Mbeki, Meles Zenawi, Olusegun Obasanjo, Abdelaziz Bouteflika na Abdoulaye Wade.
Mkapa ni mume wa mke mmoja na watoto wawili; Nicodemus ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Steve sijui kazi yake. Alioa mwaka 1966 akiwa kijana wa miaka 28. Alimuoa Anna Joseph Shauri Maro wakati huo mtumishi wa wizara ya habari, aliyesomea Uingereza. Ndoa yao ilifungwa ukweni Moshi katika kanisa katoliki. Mkapa alibaki kuwa mkatoliki kwa maisha yake yote na Anna ameendelea kuwa mlutheri hata sasa kwa sababu walipendana kwa dhati.
Halafu Mkapa alisikiliza sana mawazo ya mke wake pengine ndo maana alifanikiwa maana wanawake ni wabeba maoni. Wakati mwingine wajumbe wamekushughulikia kwa sababu hukumshirikisha mkeo kwamba unatia nia akakuombea!
Wazo la Mkapa kugombea Urais lilianzia kwa Jenerali Ulimwengu na vijana wenzake waliokuwa bungeni enzi hizo, wazo likaenda kwa Mzee Warioba na kufika kwa Mkapa, Mkapa akalipeleka kwa wife, theni kwa jamaa zake na mwisho kwa Mzee Nyerere. Nyerere alishangaa lakini akakubali kumuunga mkono ingawa alikuwa na mgombea wake, Salim Mohammed Salim.
Wengi walipigwa butwaa siku Mkapa alipochukua fomu. Jamaa hakuwa na umaarufu kwa sababu aliishi sana nje, lakini pia hakuwa msemaji sana hadi Augustine Mrema akamwita "Bubu". Kuna magazeti yaliandika kwamba Ken Mkapa wa Yanga alijulikana zaidi Tanzania kuliko Mkapa. Kwenye kampeni za Mkapa, Jenerali Ulimwengu alikuwemo, sema walikuja kuzinguana baadaye!
Nimalizie kwa kusema, Mkapa alikuwa mtu wa matani na vichekesho pia. Hata ule upara alisema ulitokana na kubeba vyombo shuleni. Shuleni walijipikia. Anasema alipokuwa chuoni watoto wa kike walimzimia kishenzi kwa sababu alijenga hoja.
The Big Ben amelala lakini fikra zake ziko macho ndo maana tunamuita hayati na siyo marehemu. Ukifa bila kuacha alama unaitwa Marehemu, ukiacha alama na fikra zinazoishi unaitwa Hayati! Enzi za uhai wake Magufuli anasema Mkapa alipinga wazo la kuzikwa Ikulu. Amerudishwa kwao baada ya kufa kwa ugonjwa wa malaria na moyo kusimama ghafla!
Pumzika kwa Amani the Big Ben!
TAZAMA MAKALA YA VIDEO HAPA>>
Comments
Post a Comment