Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Joseph Nyamhanga, amemwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Spora Liana, kuhakikisha mabasi yaendayo mikoani yanahamia katika kituo kipya cha mabasi Mbezi Luis, kabla ya Oktoba 15, mwaka huu.
Nyamhanga alitoa agizo hilo juzi baada ya kutembea kituo hicho cha mabasi, kwa ajili ya kukagua maendeleo ya mradi huo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 77.
lisema Halmashauri ya Jiji hilo, inapaswa kuhakikisha ujenzi huo unakamilika katika muda uliopangwa ili kuanza kwa utekelezaji kama ambavyo imepangwa.
“Mkurugenzi hakikisha mabasi yote ya mikoani yanahamia hapa kabla ya Oktoba 15 muda ambao mmepanga mradi uwe umekamilika,” alisema Nyamhanga.
Alisema mabasi hayo yanapaswa kuhama kutoka kituo cha mabasi Ubungo ili kupisha eneo hilo kwa ajili ya kuwa Karakana Kuu ya Mabasi ya Yaendayo Haraka.
Alisema eneo hilo lilipaswa kuwa limeshakuwa wazi kwa ajili ya kuwa karakana ya mabasi hayo, lakini kutokakamilika kwa mradi huo wa kituo cha mabasi cha Mbezi Luis kwa wakati kumesababisha kutotekelezwa kwa mpango huo.
“Nimewaagiza na naendelea kuagiza kuwa, miradi yote ya kimkakati kama hiki kituo cha mabasi naomba niwe napewa ripoti ya maendeleo yake kila mwezi,” alisema Nyamhanga
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa jiji hilo, Liana aliahidi kuwa mradi huo utakuwa umekamilika Oktoba mwaka huu na matarajio yao kuhakikisha mabasi yote yanahamia katika kituo hicho kabla ya Oktoba 15, kama ambavyo wameagizwa na Katibu Mkuu.
Alisema mradi huo unagharimu Sh. bilioni 50.94, na kwamba utakapokamilika unatarajia kuliingizia jiji hilo mapato ya Sh. bilioni 7.2 kwa mwezi.
Alisema hadi sasa katika mradi huo wameshatumia shilingi bilioni 20.46, na kwamba wanaweza kutumia chini ya gharama zilizopangwa na fedha zitakazobaki watazitumia katika shughuli nyingine za kuboresha kituo hicho.
Liana alisema mradi huo ulitakiwa uwe umekamilika kabla ya Julai mwaka huu, lakini umechelewa kwa sababu ya kuwapo kwa ugonjwa wa COVID-19 na uzembe wa mkandarasi ambaye hata, hivyo wameshambadilisha.
“Mradi huu umechelewa kwa sababu ya kuwapo kwa ugonjwa wa COVID-19 ndipo mkandarasi alisimamisha vibarua wote hali iliyochelewesha kukamilika kwa mradi ingawa tayari alishaanza kazi tangu Rais John Magufuli alipoagiza Watanzania kuendelea na shughuli za kila siku,” alisema Liana.
Alisema pia licha ya kukamilisha mradi huo kwa wakati kama ambavyo wameagizwa, kuna changamoto ya ujenzi wa barabara ya kuingilia kituoni hapo inayotakiwa kujengwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).
Sambamba na hilo, alisema malengo ya jijini hilo ni kujenga hoteli na mabweni ya kufikia wageni wanaotaka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi katika awamu ya pili ya mradi huo.
Comments
Post a Comment