Mr Kuku Anaswa Kwa Kuchezesha Upatu Wa Mabilioni Ya Fedha

 Mfanyabiashra na Mkazi wa Oysterbay jijini Dar es Salaam, Tariq Machibya miaka (29) maarufu kama Mr Kuku, akiwa kortini Kisutu kusubiria kusomewa kesi inayomkabili.

Mfanyabiashra na Mkazi wa Oysterbay jijini Dar es Salaam, Tariq Machibya miaka (29) maarufu Mr Kuku, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

 

Mshtakiwa amesomewa mashtaka yake leo Agosti 10,2020 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Godfrey Isaya.

 

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Wankyo amedai mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 60/2020 ambapo katika mashtaka hayo saba yanayomkabili mshtakiwa huyo, yapo ya  kusimamia na kuendesha biashara haramu ya upatu; kupokea maingizo ya fedha kutoka kwa umma bila kuwa na leseni na mashtaka matano ni kutakatisha fedha.

 

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kati ya Januari 2018 na Mei 2020, katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam, mshtakiwa anadaiwa kusimamia biashara ya upatu.

 

Pia anadaiwa kujihusisha na biashara ya upatu kwa kukubali na kukusanya fedha kutoka kwa umma, akijifanya kwamba watafanya ujasiliamali wa ufugaji wa kuku na wangepata faida ya asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa kipindi cha miezi sita, kiasi ambacho ni kikubwa katika biashara kuliko mtaji uliokusanywa.

 

Wankyo amedai  kati ya April 26, 2019 na Januari 26, 2020 maeneo ya Jiji la Dar Es Salaam, alijihusisha na miamala ya Sh 6.4bilioni kwa kutoa fedha hizo kutoka katika akaunti inayosomeka kwa jina la Mr Kuku Farmers Ltd iliyopo katika benki ya CRDB, wakati akijua kuwa fedha hizo ni zao tangulizi la biashara haramu ya upatu.

 

Upande wa mashtaka umedai kuwa kesi niya uhujumu uchumi na upelelezi katika shauri hilo haujakamilika na Hakimu Isaya ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 24, mwaka huu.


Chanzo:GlobalPublishers

Comments