Simbachawene Aagiza Polisi Kuwadhibiti Wanasiasa Watakaoleta Vurugu Uchaguzi

 


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amevionya vyama vya siasa nchini ambavyo vina wagombea katika ngazi mbalimbali vizingatie sheria kwa kuhakikisha wanachokifanya hakileti uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha uchaguzi.

 

Pia amelitaka Jeshi la Polisi nchini kusimamia amani na utulivu, kuanzia Polisi Kata, Wilaya mpaka Mkoa kuwathibiti watu watakaoleta fujo na wasisubiri mpaka Inspekta Jenerali wa Polisi aseme.

 

Akizungumza katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Kigoma, kabla ya kuanza ziara katika makambi ya Wakimbizi Mkoani humo, Simbachawene alisema mtu yeyote, chama chochote kitakacholeta vurugu lazima adhibitiwe.

 

“Lazima sheria ifuatwe, hatufanyi uchaguzi kama sisi ni wanafunzi wa uchaguzi, sisi watanzania katika ukanda huu tumefanya uchaguzi wa demokrasia mara nyingi kuliko nchi yoyote, haiwezekani tukasikia watu bado wanakufa kwenye harakati za uchaguzi, nchi hii inamaana zaidi kuliko hiyo unayoifikiria siasa,” alisema Simbachawene.




Comments