TCRA: Zingatieni Kanuni Mpya Za Maudhui Mtandaoni Za 2020

 

Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa,MhandisiFrancis Mihayo amevitaka Vituo vya Utangazaji (Radio,Televisheni,Blogs na Online Tv) kuzingatia Kanuni mpya za Maudhui Mtandaoni mwaka 2020 na Kanuni Mpya za Redio na Televisheni mwaka 2020 ambazo tayari zimeanza kutumika mwezi Julai,2020. 

Mihayo ameyasema hayo wakati wa kikao kati ya TCRA na Vituo vya Utangazaji (Radio,Televisheni,Blogs na Online Tv) Kanda ya Ziwa ambacho pia kimehudhuriwa na Wenyeviti wa Klabu za waandishi wa habari (Press Clubs) na waandishi wa habari wa vituo hivyo, kilichofanyika leo Jumatatu Agosti 10,2020 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza. 


Mihayo ameyasema hayo wakati wa kikao kati ya TCRA na Vituo vya Utangazaji (Radio,Televisheni,Blogs na Online Tv) Kanda ya Ziwa ambacho pia kimehudhuriwa na Wenyeviti wa Klabu za waandishi wa habari (Press Clubs) na waandishi wa habari wa vituo hivyo, kilichofanyika leo Jumatatu Agosti 10,2020 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza. 

Kikao hicho kilichoandaliwa na TCRA kwa kushirikiana na Chama Cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kililenga kukusanya maoni ya wadau yatakayotumika kwenye marekebisho ya Kanuni za hakimiliki,uwasilishaji mada za namna ya kuripoti wakati wa Uchaguzi mkuu na marekebisho ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za 2020. 

Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi Mihayo alisema Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya Habari na Utangazaji imetoa maboresho ya Kanuni za maudhui mtandaoni zijulikanazo kama “THE ELECTRONIC AND POSTAL COMMUNICATIONS (ONLINE CONTENT) REGULATIONS,2020” ambapo Kanuni hizo zimelenga kuboresha huduma za maudhui mtandao na usimamizi wake kutokana na uzoefu uliopatikana kwa kipindi cha miaka miwili toka Kanuni za zamani zilipoanza kutumika mwaka 2018. 

Mhandisi Mihayo alisema TCRA Kanda ya Ziwa imeamua kukutana na Vituo vya Utangazaji ili kutoa elimu kuhusu maboresho ya kanuni hizi ni kuwasaidia watoa huduma za maudhui kwa tayari mabadiliko kwenye kanuni za maudhui ya kimtandao za mwaka 2020 zilizoanza kutumika Julai Mosi, 2020.


Mkuu huyo wa TCRA Kanda ya Ziwa,alisema Kati ya maboresho muhimu yaliyofanyika kwenye Kanuni za mwaka 2018, na kuingizwa kwenye Kanuni mpya za maudhui mtandao mwaka 2020 ni pamoja na Mgawanyo wa makundi ya leseni mtandaoni. 

Alitaja makundi hayo kuwa ni Leseni za maudhui mtandaoni kwa ajili ya Habari na Matukio (News and Current Affairs), Leseni za maudhui mtandao kwa ajili ya waburudishaji kama vile filamu, muziki, vichekesho, cartoon, drama n.k (entertainment), Leseni za maudhui mtandao kwa ajili ya utoaji elimu tu (education programmes) na Leseni za maudhui mtandao kwa ajili ya maudhui ya dini (religious content). 

“Kwa kuzingatia uzoefu uliopatikana kwa miaka miwili, Kundi la watoa huduma za maudhui ya elimu na dini limepunguziwa gharama za leseni na malipo ya kila mwaka kwa asilimia 50%. Kutoka fedha ya Kitanzania Shilingi Milion moja (1,000,000/=) mpaka laki tano (500,000/=). Punguzo hilo limelenga kuwafanya watanzania wengi washiriki kutoa huduma za maudhui mtandao bila kuvunja Sheria”,alisema Mhandisi Mihayo. 

Alisema Kanuni mpya za maudhui mtandaoni mwaka 2020 zimeweka vifungu vya maelekezo ya kuwalinda watoto na kuzuia maudhui yasiyofaa mtandaoni.

"Baadhi ya maudhui yaliyozuiliwa kuingia mtandaoni ni pamoja na maudhui ya ngono, maisha binafsi ya mtu na kuheshimu utu wa mtu, usalama wa taifa na ukiukwaji wa sheria, biashara haramu, afya na usalama wa raia, haki miliki, dini na taarifa za uchochezi zinazoweza kuvuruga amani",alisema. 

Aidha kwa upande wa adhabu kwa wenye leseni za kutoa huduma mtandaoni, alisema adhabu kwa wenye leseni za kutoa huduma za maudhui mtandao zimefafanuliwa na kuongeza adhabu zingine ambazo ni sasa mtoa huduma mtandaoni atapewa Onyo kali,Kuomba msamaha kutumia vyombo vya habari na kuamriwa kuondoa maudhui yasiyofaa. 

Katika hatua nyingine Mihayo alivitaka Vituo vya Utangazaji vinavyojiunga na vyombo vya habari vya nje kuomba kibali TCRA ili kupatiwa kibali cha kujiunga na vyombo vya nje ili kuendelea kupokea matangazo. 

Mkuu huyo wa TCRA Kanda ya Ziwa alisema mpaka sasa Kanda ya Ziwa kuna Vituo viwili vya Televisheni,Redio 40 na watoa huduma mtandaoni 18 (Blogs & Online Tv). 

Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi TCRA Kanda ya Ziwa,William Mnyippembe alivikumbusha vyombo vya habari vitakavyokuwa vinaripoti masuala ya uchaguzi mkuu 2020 kuhakikisha vimesajiliwa na TCRA na kufuata sheria,taratibu na kanuni zilizowekwa.

"Katika kipindi cha uchaguzi mwajiriwa yeyote wa kituo cha utangazaji anayetaka kujihusisha na siasa, ni lazima aende likizo, aache kazi ama apumzike wakati wa mchakato wa uchaguzi.


"Utoaji taarifa siku ya uchaguzi ni lazima vituo vya habari vihabarishe kile walichokiona, wasitegemee taarifa za kuambiwa ama maoni yao bali kile walichokiona eneo ambalo kura zinapigwa, pia waepuke kutoa mambo ambayo ni ya kufikirika na taarifa zenye kusudi la kuchafua mtu",alisema Mnyippembe. 

Afisa Mawasiliano wa TCRA Makao Makuu, Herieth Shija, akiwasilisha mada juu ya maboresho ya kanuni mpya za matangazo ya Redio na Television ya mwaka 2020, alisema miongoni mwa maboresho yaliyofanyika ni vipindi vya watu wazima visivyopaswa kusikilizwa na watoto vianze kuruka kuanzia saa 6 usiku hadi 11 alfajiri tofauti na hapo awali vilipokuwa vinaruka kuanzia saa 4 usiku.

Naye Mwanasheria kutoka COSOTA, Lupakisyo Mwambinga akiwasilisha mada kuhusu Mapendekezo ya Kanuni Mpya za Utangazaji,Maonesho na Mawasiliano kwa umma zilizotungwa chini ya Sheria ya Hatimiliki na Hakishirikishi sura ya 218,aliwataka kutunza kumbukumbu za nyimbo wanazopiga kwenye vyombo vya habari ili kanuni zinapoanza kutumika wasipate tabu.
PICHA NA:Kadama Malunde

Comments