Waziri BITEKO: Rais Magufuli Anataka Wachimbaji Kunufaika Na Rasirimali Madini

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anataka wachimbaji wote wa madini nchini wafaidike na madini ambayo Mwenyezi Mungu amewabariki kuwanayo katika maeneo yao.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko, alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi wilayani Kyerwa Mkoa wa Kagera ambapo alizungumza na wachimbaji pamoja na wafanyabiashara wa  Madini ya Bati (Tin).

Waziri Biteko alisema, anachokitaka Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni kuona wachimbaji wote wa madini nchini wanafaidika na madini yaliyopo kwenye maeneo yao, hii ndiyo awamu ya wachimmbaji kutajirika.




“Wote ni mashahidi kwa muda mrefu madini yetu yalikuwa yanatoroshwa, lakini Mheshimiwa Rais akasema hapana tuanzishe masoko, leo wote tunaona mafanikio makubwa yanayotokana na masoko hayo,” alisema Waziri Biteko.

Tanzania hatukuwahi kuwa na Cheti cha Uhalisia wa Madini ya Bati lakini Rais akasema hapana tutafute Cheti cha Uhalisia lakini tunashukuru Mungu Cheti cha Uhalisia tumekipata, Biteko aliongeza.

Aidha, Waziri Biteko amewaruhusu wafanyabiashara wa Madini ya Bati kuyasafirisha madini yaliyoongezwa thamani kwenda kuuzwa nje ya nchi ili yauzwe kwa bei nzuri na wachimbaji kufaidika.

Pamoja na mambo mengine Waziri Biteko, amewataka wachimbaji wa Madini ya Bati kurejea kazini na kuachana na vitendo vya kutorosha madini hayo na badala  yake wayapeleke sokoni.


PICHA NA: Kadama Malunde

Comments